Kati ya kitu ambacho kinatafutwa sana na watu wengi ni kujisikia vizuri. Kwa sababu ya matamanio haya ya kutaka kujisikia vizuri, matokeo yake watu wengi wamekuwa wakijihusisha na mambo ya hovyo sana.
Kwa mfano, kwa sababu tu ya kutaka kujisikia vizuri (feel good) watu wamekuwa wakifanya vitu kama uvutaji wa sigara, kufanya mapenzi na wanawake wengi au kinyume cha maumbile ili kupata tu ile radha ya kujisikia vizuri.
Lakini pamoja na kufanya yote hayo, bado ridhiko kamili na kudumu la kujisikia vizuri linakuwa halipo, kwa sababu starehe hizo hupelekea shida nyingi na magonjwa kama ukimwi au uathirika wa dawa za kulevya.
Wasichokijua wengi, kujisikia vizuri, hakutokani na mambo ya nje, bali kunatokana na jinsi unavyoweza kutawala hisia zako.
Ukishindwa kutawala hisia zako, hata ufanye nini, hutajisikia vizuri moja kwa moja, ni kwa muda tu.
Ukiweza kutawala hisia zako vizuri, kaa ukijua utajisikia vizuri tu, hata bila kutumia sigara inayounguza mapafu, au kufanya mapenzi hovyo ambako kunaweza kukupa ukimwi na magonjwa mengi.
Ukikaa ukachunguza, utagundua watu wengi wameharibu sana, afya, maisha yao, kwa sababu ya matamanio ya kutaka kujisikia vizuri.
Kuwa makini na yale unayotaka kufanya hasa unapotaka kujisikia vizuri. Kama unafikiri natania, waulize wenye wanawake au wanaume wengi. Waulize wanaovuta sana dawa za kulevya, kile walichokuwa wakikitafuta wamekikosa, wengi wameambulia uathirika na magonjwa.
Na: Imani Ngwangalu

0 Comments