Ukiamaka asubuhi, kitu cha kwanza huwa kina kuwa ni nini? Je huwa anaanza kushika simu na kuangalia ni nani alaiyekutafuta? Au huwa anaanza kuangalia kwenye mitandao ya kijamii ni habari gani iliyokupita?
Kama jibu ni ndiyo, basi kuna mahali unakosea kwa sababu unaweza kuanza na mambo hayo ambapo wakati mwingine yanaweza kutakutoa kwenye mudi uliyonayo. Hiyo ni kwa sababu unaweza kukutana na habari ya kusikitisha ambayo hukuitegemea.
Sasa wataalamu wa mambo wanasema siku njema huonekana asubuhi, hii ikiwa endapo mwenye umiliki wa asubuhi hiyo ataianza siku yake vizuri.
Na ili uweze kuianza asubuhi yako vizuri pasipo kuwa na bugudha ya aina yeyote ile haya ndiyo mambo ya msingi ya kuzingatia kila unapoamka asubuhi;
1. Mambo ya kiimani.
Unapoamka asubuhi na mepema unatakiwa kumtangukizia muumba wako kabla ya kuianza siku yako kwa kufanya haya yafuatayo;
Kwanza unatakiwa kumshukuru Mungu kwa kukuamsha salama, kwa sababu kukuamsha salama ni baraka tosha kwani wapo baadhi ya watu hawajaamka toka walivyolala.
Pili unatakiwa pia umuombe mwenyezi Mungu akawe baraka yako katika siku yako ambayo unakwenda kuianza. Siku yako ikawe yenye baraka na pia muombe Mungu aibariki kila kazi ya mikono yako utakayokwenda kuitenda kwa siku husika.
2. Mambo ya kiafya.
Kila unapoamka asubuhi yapo masuala ya kiafya unayotakiwa kuyafanya, ikiwa ni pamoja kufanya mazoezi walau hata kwa dakika kadhaa ili uweze kuweka mwili wako vizuri, hii ni kwa sababu watalamu wanasema mazoezi huleta afya ya mwili pia wakati mwingine huzuia baadhi ya magonjwa nyemelezi.
Pia kila ukiamka asubuhi unatakiwa kunywa maji kwa ajili ya kuweka mwili wako vizuri pia, watalamu wa afya wanasema asilimia 75 ya mwili wa mwadamu hutegemea zaidi maji ambayo yapo mwilini, kama ndivyo hivyo zipo faida lukuki utakazozipata endapo utakuwa na utaratibu wa kunywa maji kila siku asubuhi.
Vile vile unapaswa kufanya usafi wa mwili na kinywa chako pia, Kila siku asubuhi weka utaratibu wa kuoga ili kufanya mwili wako uwe safi na nadhifu. Pia watalamu wa afya wanashauri kama mwili wako hauna tatizo lolote la kiafya ukioga maji ya baridi ni vizuri zaidi.
Pia kumbuka kusafisha kinywa chako vizuri kwa kupiga mswaki mara baada ya kupata kifungua kinywa kama una utaratibu huo wa kupata kifungua kinywa.
Nb; kupiga mswaki kunapaswa kufanyika kila baada ya kupata chakula chochote kile, hata kwenye vifungashio vya dawa za meno kumeandikwa maneno hayo.
3. Mambo yako binafsi.
Kila unapoamka asubuhi pia ni wakati wako mzuri kufanya tafakari juu ya maisha yako. Waza namna bora siku yako itakavyokuwa. Waza namna utakavyokwenda kufanya majukumu yako kwa mpangilio ulio sahihi.
Pia unatakiwa kuhakikisha unakamilisha kila jukumu ulilopanga kulifanya kwa siku husika kabla hujaanza kufanya jukumu jingine. Kurukaruka katika kufanya kazi kuna kufanya upoteze uelekeo sahihi wa majukumu yako.
Hayo ni mambo muhimu sana unayotakiwa kuyafanya kila ukiamka asubuhi, ukifanya hivyo kila siku, siku yako itakuwa ni njema sana yenye baraka na mafanikio tele ndani yake.
Ndimi; Afisa Mipango Benson Chonya.
.png)
0 Comments