Kwenye maisha haya tunayoyaishi mimi na wewe tunapaswa kuwa makini sana na vile ambavyo tunaishi na watu wengine.
Kwa sababu wengi tunapenda kuwashirikisha watu wengine matatizo yetu hata wale wasiyohusika. Kitendo hicho hutuaminisha kwamba huenda wale tuliowashirikisha wangetusaidia ila kitu cha kushangaza mambo huwa yapo kinyume chake.
Yafuatayo ndiyo mambo ambayo hutakiwi kuwashirikisha watu wengine;
Usiwashirikishe watu ndoto zako.
Watalamu wa mambo wanasema usipende kuwashirikisha watu ndoto zako kwa sababu wewe ndiye mwenye picha kamili ya kile unachokitaka.
Watu wengine hawaioni picha hiyo kamili ya ndoto yako, hivyo ukiwashirikisha, wengi wao watakwambia hilo jambo haliwezekani, hivyo kwa kuwa wewe unawaamini zaidi wao unajikuta unachaana na kile unachokiamini na kuamini kwenye mawazo yao.
Ukubwa wa picha kamili ya kile unachokiona katika ndoto yako wewe ndiye ambaye unakiona hivyo, hivyo unatakiwa kupambania ili kile unachokiona kiweze kutimia.
Usiwashirikishe watu ndoto zako bali waonyeshe kwa vitendo mafanikio yako watu hao.
Usiwashirikishe watu matatizo yako.
Usipende kuwashirikisha watu matatizo yako kwa sababu si kila mtu atakuwa pamoja na wewe katika matatizo yako, bali watu wengine hugeuka ubao wa matangazo, kwani wao watakuwa wanatangaza kwa watu juu ya matatizo unayoyapitia.
Utawasikia wakisema usimuone hivyo alivyo, hivi hapo alivyo ana matatizo chungu mzima. Hao ndiyo binadamu, unaweza sema ni mwema kwako kila upitiapo matatizo bali yeye hugeuka kuwa chanzo cha kuyasambaza yale unayoyapitia kwa watu wengine.
Nb; Tafuta watu wachache sana wa kuwashirikishe yale magumu unayoyapitia, iwe mvua liwe jua wao hawataweza kukusambazia kwa watu wengine magumu yako.
Usiwashirikishe watu kuhusu kipato chako unachopata.
Epuka kuwaambia watu kuhusu kipato chako kwa sababu unapowaambia watu wengine kuhusu kipato chako, watu hao watajua wao wakuweke kwenye kundi gani.
Watu hao wataanza kuwaambia usimuone hivyo alivyo kumbe kwa mwezi analipwa kiasi cha shilingi elfu arobain tu, wengine watasema usimuone ana kazi nzuri, mshahara mzuri ila huwezi amini hata nyumba yake hana, amepanga tu.
Narudia kusema usiwaambie watu kipato chako ili uwapunguzie watu kukujadili. Watu wakijua kipato chako muda mwingi watakuwa wanakujidili wewe, kwa kulinganisha maisha yako ni kipato chako.
Usiwashirikishe watu matatizo yanayoikumba familia yako.
Jambo jingine ambalo hutakiwi kuwaambia watu ni kuhusiana yale magumu yanayotokea katika familia yako. Kama nilivyosema hapo awali ya kuwa wapo baadhi ya watu hugeuka ubao wa matangazo kwa kusambaza yale mnayoyapitia katika familia yako endapo utawashirikisha mambo hayo.
Hivyo kuwa makini sana kwenye hilo, mambo ya kifamilia basi yajadiliwe ndani ya familia kwa sababu kama mambo hayo yatatoka nje ya familia husababisha watu wengine wayajadili yale yote yaliyotokea ndani ya familia yenu hata kama mambo hayo hayawahusu.
Mpaka kufikia hapo sina la ziada nikutakie siku njema na utekelezaji mwema.
Ndimi afisa mipango Benson Chonya.
0747030303
.png)
0 Comments