BREAKING ARTICLES

6/recent/ticker-posts

Mafanikio ni mchakato

 


Tunaishi katika ulimwengu ambao watu wake  wamechoshwa na hali ya maisha wanayoishi, wengi wao wanataka watoke kutoka hali moja kwenda hali nyingine kwa maana ya kupata mafanikio wayatakayo.

Pamoja na shauku na nia yao hiyo waliyonayo, ila wengi wanategemea kupata mafanikio ya haraka zaidi, kuliko mafanikio yenyewe yanavyotaka. Wengi hawataki kuchelewa, wengi wanataka waanzishe kitu leo kianze kuwalipa siku hiyo hiyo.

Wengi wamesahau kuwa mafanikio ni mchakato. Kama ilivyo kwa upatikanaji wa mtoto kwamba haiwezekani  na haitakuja kuwezekana mtu apate mimba leo na azae siku hiyo hiyo, bali kuna mchakato wake mpaka mtoto apatikane, mchakato huo ambao kila mtu anaujua.

Au kama ulivyo mchakato wa uotoaji wa mbegu yeyote ile ya mmea kwamba ni lazima uchukue kipindi cha muda fulani ndiyo ianze kuota, mchakato huo ndivyo ulivyo hata kwenye mafanikio ni lazima kila kitu kipite kwenye mchakato fulani ili kitu hicho kiwe kitu halisi.

Maisha ya mafanikio yanahitaji mchakato, hakuna mafanikio ya siku moja. Mafanikio siyo kama mchezo wa bahati nasibu, kwamba ni mchezo wa kulala maskini na kuamka tajiri. Kila mtu anatakiwa kupambana kila siku ili kufikia malengo yako.

Hakuna kitu ambacho utakianzisha leo kisha ukategemea kitu hicho kianze kukulipa leo leo, hilo jambo halipo. Kila kitu huchukua muda fulani ili uanze kuona matokeo ya jambo hilo.

Huwezi kwenda shule, ukasoma kila kitu au madarasa yote kwa siku moja, bali kila kitu huenda kwa hatua zake.

Ili uweze kupata matokeo chanya kwenye kila jambo usiwe na pupa ya kutaka kupata kila kitu kwa siku moja bali jipe muda huku ukiongeza juhudi za utendaji wako wa kazi kila siku ili uweze kupata matokeo tofauti na yale uliyoyapata jana.

Pia nitamatishe kwa kusema kila siku shindana na wewe yule wa jana usishindane na mtu, kwani ukishindana na kila mtu utataka mafanikio ya haraka ambayo hayana mchakato sahihi.

Imeandikwa na Afisa mipango Benson chonya.
0747030303

Post a Comment

0 Comments