Leo ndiyo siku pekee ambayo tunayo imiliki, kesho hatuna imiliki nayo, hatujui kama itafika au haitafika. Hivyo kwa kuwa siku ya leo ndiyo ipo mikono mwetu basi tuitumie vyema kuweza kufanya mapinduzi makubwa katika maisha yetu.
Kama lipo jambo tunataka kulifanya leo ni heri lifanyike leo, usiseme nitafanya kesho kwani hiyo kesho hauna umiliki nayo. Kama kuna wazo umelipata anza kulitekeleza leo kwa mfano kama unataka kuanza biashara ni afadhali ukaanza leo, kama unataka kuanza kujifunza kitu ni heri uanze leo, kama unataka kuanza kuweka akiba basi anza leo kitu chochote unachotaka kukifanya maishani ni vyema ukaanza leo.
Hata wahenga waliwahi nukuliwa wakisema " linalowezekana leo, lisingoje kesho" maana yake ni kwamba kila kitu kinachowezekana leo basi kifanyike leo.
Fanya maamuzi maishani mwako kwa kuamua kuitumia leo yako vyema. Usiwe muumini wa kusema nitafanya kesho, kesho siyo rafiki mwema wa mafanikio yako, bali matumizi sahihi ya leo yako ndiyo yenye kuleta matokeo mazuri katika maisha yako.
Watu wengi kwenye ulimwengu huu, wameamini kesho ni rafiki wa mafanikio hivyo hujikuta watu hao wanaghairi kwenye vingi. Kama na wewe ni mmoja wa watu ambao wanaaamini kwenye nachopaswa kukumbusha siku ya leo ni kwamba kesho ipo kwa ajili ya wajinga na wavivu.
Wajinga na wavivu ndiyo ambao huamini katika kesho, mara nyingi ujinga wao na uvivu wao upo kwenye kufikiri na kutenda.
Huamini wao wana muda hivyo hata uwezo wao wa kufikiri huwa upo chini kwa sababu wanaamini watafanya jambo hilo siku inayofuata.
Kitendo hicho cha kuamini kuna kesho hutupelekea wengi wetu kutofanya maendeleo huku tukiamini tuna muda wa kutosha. Ndugu yangu badilika usiwe na mtazamo wa namna huyo, anza kuishi kana kwamba hakuna kesho hivyo kila kitu kinakiwa kufanyika leo.
Kila mmoja wetu awaze namna ya kuwa bora katika maisha yake, kwa kuitumia leo yake vyema, ambayo itampa maisha bora yenye matumaini na mafanikio tele.
Ndimi Benson Chonya.
.png)
0 Comments