Tunaishi kwenye dunia ambayo ukiachana mambo mengine chuki imetawala sana. Chuki ambazo mara nyingi zimetokana na mafanikio yetu, yaani watu wamekuwa hawependi mafanikio yetu hivyo watu hao hujikuta wanatengeneza chuki dhidi yetu.
Chuki hizo hazikwepeki, zipo na zitaendelea kuwepo daima. Zipo chuki ambazo zinapatikana ndani ya familia, zipo chuki ambazo hutokana kwa marafiki zetu, zipo chuki kutoka kwa wanajamii, zipo chuki kutoka kwa watu tunaofanya nazo kazi na zipo pia chuki kutoka kwa watu ambao hatuna hata ukaribu nao.
Kwa mfano leo labda unamiliki kitu fulani, na kwa kuwa unaishi kwenye jamii yenye chuki dhidi yako utakuta idadi kubwa ya watu watajitokeza na kuanza kukuchukia tu pasipo kuwa na sababu za msingi.
Kwa mfano watu hao huanza kuumba maneno, mara ooh usimuone hivyo, hizo hela zote anazozimiliki alizipata kwa njia za kishirikina. Mara hivi usimuone anavyopendeza hivyo, hivi kazi yake ni udangaji. Yapo maneno mengi ambayo kiukweli kama utayasikia mara nyingi huwa yanatia kinyaa.
Hivyo ndivyo dunia ilivyo watu wamejawa na chuki sana. Watu wengine wanapenda kuona ya kuwa hatufikii malengo yetu fulani, wanapenda kuona tunabaki kuwa kama wao, wanapenda kuona tunaishi maisha ya chini zaidi ya yale wanayoishi wao, na kitendo hicho ndicho ambacho huzalisha chuki.
Chuki ambazo kama utakuwa mtu ya kuyumbishwa na chuki hizo zinaweza kukuathiri kwa namna moja ama nyingine katika utendaji wako wa kazi. Chuki huzalisha maneno ambayo yanaumiza sana, maneno ambayo kama utaamua kuyabeba kama yalivyo huwa yana athari kubwa sana katika maisha yako.
Sasa ikiwa unaishi na watu wenye chuki dhidi yako unatakiwa kufanya yafuatayo;
1. Kuwa mtu mwenye tabasamu muda wote.
Wetu wengi wenye chuki dhidi yako huwa wana matarajio fulani kutoka kwa kwako. Kwa mfano wanaweza kusambaza maneno mabaya dhidi yako ili maneno yale yakuchukize.
Kwa kuwa wao matarajio yao ni kuona wewe unachukia basi wewe jitahidi kila unapokutana na watu hao wewe huchukii bali waonyeshe tabasamu mwananana ili kile ambacho walitegemea kutoka kwako kiwe ni kinyume chake.
Ukifanya hivyo ni lazima watashangaa tu, kuwa imekuwaje? Mbona walitegemea kwamba utakuwa na chuki dhidi yao ila cha kushangaza wewe hauna chuki hiyo waliyoitegemea?. Hapo ni lazima wao wenyewe watajirekebisha na kuona walichokifanya siyo kitu sahihi hivyo chuki hiyo itaanza kuondoka kwao taratibu.
2. Acha vita ya maneno waonesha mafaniko yako kwa vitendo.
Jamii tunayoishi kama nilivyosema hapo awali kwamba imetawaliwa na chuki, chuki ambayo chanzo chake ni maneno, kama ndivyo hivyo pale unaposikia maneno ya aina fulani yenye chuki dhidi yao, basi usiwajibu tena watu hao kwa maneno kwa sababu ukiwajibu kwa maneno chuki hiyo haitaisha bali utazalisha kitu kinachoitwa vita ya maneno.
Kitu pekee unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unawaonesha hao watesi wako mafanikio yako kwa vitendo. Yaani kila siku usiwajibu kwa maneno bali endelea kupambania ndoto zako kwa vitendo, kuwajibu kwa maneno kwa yale wanayoyasema ni kuwapa nguvu ya kuendelea kusema, kuwajibu kwa maneno kitendo hicho kitasababisha upunguze umakini wako kwenye kazi zako.
Kuwanaonesha mafanikio yako zaidi hii ni njia bora zaidi ya kuwandoa watu wenye chuki dhidi yako, kwani wao wenyewe watashtuka na kusema mbona pamoja na yote hayo ila mbona bado mtu huyu unafanikiwa?. Hapo wao wenyewe wataanza kutoa chuki zao dhidi yako.
3. Wasemehe bure.
Mara baada ya kuwaonesha watu hao mafanikio yako kwa vitendo, unatakiwa uwasamehe kwa kile wanachokifanya dhidi yako. Usiishe kuwasemehe tu bali kile wanachokisema kipuuze pia.
Pia ni muhimu sana kuwaseheme wale wenye chiki dhidi yako kwa sababu unapomsahe mtu unapunguza pia hata muda wa kumfikiria yeye. Na unaanza mara moja kuwaza mambo yako na unaachana na hicho alichokisema dhidi yako.
Ukitumia njia hizo ni kwamba watu hao wenye chuki dhidi yako, watatoka kwenye kile kilichofanya wakuchukie kwa sababu wataona kuwa vita ambayo wameianzisha haina majibizano tena.
Kwa nukta hiyo, nikutakie siku njema na mafaniko mema. Asante.
Ndimi afisa mipango Benson Chonya.
0747030303
.png)
0 Comments