Ipo nguvu kubwa sana ya maneno ambayo mara nyingi huwa tunajiambia sisi wenyewe. Maneno haya yanaweza kuwa ni yale ambayo ni kujenga au maneno yale ambayo ni ya kubomoa.
Ila leo nitazungumzia zaidi maneno hasi ambayo huwa tunajinenea ambayo mara nyingi yamekuwa yakitufelisha kwenye vitu sana katika maisha yetu.
Watu wengi sana tumekuwa tukiyapuuzia mawazo yetu ambayo huwa yanatujia akili mwetu kwa kujinenea yale yaliyo mabaya zaidi ambayo hutufanya tuzidi kurudi nyuma kwenye maisha yetu ya kila siku.
Kwa mfano unaweza ukawa umekaa pekee yako mara ghafla likajia wazo fulani zuri tu, ila wewe ukawaza mawazo hasi juu ya wazo hilo. Kwa mfano unaweza waza labda ufungue biashara ya nguo sehemu, baadala ya kutulia kwenye namna ya kulitekeleza wazo hilo katika ubora, ghafla unajiambia hili wazo haliwezekani mbona fulani alifanya na halikuwezekana.
Mwisho wa siku kushindwa kwa mtu fulani kunakufanya ujinenee yaliyo hasi kwamba haiwezekani.
Huo ni mfano tu ila ukweli ambao upo wazi ni kwamba wengi wetu hutumia muda mwingine kujinenea maneno hasi ambayo hutukatisha tamaa sana. Maneno ambayo hutafanya tujione haya maisha ni ya watu wachache.
Pia maneno hayo yametufanya tujione hatuwezi kabisa kuweza kufanya mapinduzi katika maisha yetu. Maneno ambayo kimsingi yametufanya maisha yetu yawe yale yale kila siku.
Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu hao ambao hujinenea yaliyo hasi kila wakati basi unatakiwa kufanya mambo haya yafuatayo;
1. Vitoe vile vyote vilivyo hasi ambavyo vipo ndani yako.
Maisha ni mkusanyiko wa herufi B na D. Neno B husimama badala ya Birth (kuzaliwa). Na neno D husimama badala ya Death (kufa). Sasa linapokuja suala la kujinenea yale yaliyo mema basi jifunze kutumia herufi B ( kuzaliwa).
Kwenye hili unatakiwa kubadili mtazamo wako wa kujifunza yale yaliyo mema zaidi, ambayo yatakufanya mtazamo wako uweze kubadilika.
Zalisha mambo mapya kwenye ufahamu wako. Miongoni mwa mambo unayopaswa kuzalizalisha ni pamoja na kuamini ya kuwa jambo fulani linawekana.
Pili itumie herufi D (death) kwa kuua au kutoa kila imani hasi iliyojengeka ndani mwako kuhusu jambo fulani. Kwa mfano kama ulikuwa huamini kuwa jambo fulani haliwezekani basi litoe jambo hilo ndani mwako na anza mara moja kuamini kuwa jambo hilo linawezekana.
2. Anza kubadili mawazo kuwa vitu.
Ili uweze kuondokana na tatizo hili la kujinenea mabaya, unatakiwa uanze mara moja kubadili mawazo yako kuwa vitu halisi kwa sababu kujinenea vibaya hutokana na mawazo, mawazo ambayo mara nyingi huwa tunayapuuzia sana.
Watalaamu wa mambo wanasema kuwa thought are things hii ikiwa na maana ya kwamba mawazo ni vitu, na kwa kuwa kila kitu kimetokana na wazo fulani hivyo tukiwa na utamaduni wa kubadili mawazo kuwa vitu tutaondokana na ile dhana ya kujinenea yale yale yaliyo mabaya ambayo huwa yanatuamisha kuwa vitu haviwezekani, na mwishone tutajenga imani kuwa vitu vinawezekana kwa sababu tumedili mawazo kuwa vitu halisi.
3. Kaa na watu wenye mtazamo chanya.
Ipo nguvu kubwa sana ya kukaa na watu wenye mtazamo chanya, unapaswa kukaa na watu wenye mitazamo chanya kuhusu jambo fulani.
Kama utakaa na watu wenye mtazamo chanya utajikuta mara nyingi hata wewe umeanza kuwa na mtazamo huo, hii kwa sababu vitu vizur vina tabia ya kujivuta vyenyewe.
Hivyo kitendo hiki cha kukaaa na watu hawa utajikuta pia unajinenea yale yaliyo chanya.
Ila kama unataka kuendelea kuwa ni mtu ambaye unataka uendelee na tabia hii ya kujinenea yale yaliyo mabaya basi endelea kukaa na watu wenye mtazamo hasi, hawa wataendelea kukuambukiza mitazamo yao, na hata ukikaa peke yako utaendelea kujinenea kile walichokuambia.
Kumbuka, kujinenea maneno chanya huleta mabadiliko makubwa sana maishani endapo muhusika atatambua thamani ya maneno hayo.
Niweke nukta kwa kusema kila wakati jifunze kujinenea yale yaliyo chanya kwa sababu yana nguvu sana ya kubadili mtazamo wako na maisha yako kiujumla.
Mpaka wakati mwingine tena, nikutakie siku njema na utekelezaji mwema.
Ndimi Afisa Mipango Benson Chonya.
0747 030303
.png)
0 Comments